AGANO JIPYA

AGANO JIPYA

Masomo
Katika somo la 2 tulijifunza jinsi dhambi ilivyoingia ulimwenguni. Kwasababu Mungu aliwapenda wanadamu, aliamua kumtuma Mwokozi duniani awezaye kuwaokoa watu katika dhambi zao. Haukuwa mpango wa Mungu kwamba Mwokozi huyo azaliwe mara bali baada ya utimilifu wa wakati (Wagalatia 4:4). Mtu mmoja wa zamani zile aliyempendeza sana Mungu alikuwa Ibrahimu. Mungu alifanya agano na Ibrahimu akimwahidi mambo matatu: (1) kwamba taifa kubwa litatoka kwake, (2) kwamba uzao wake watapewa nchi ya Kanaani, na (3) kwamba katika yeye jamaa zote za dunia watabarikiwa kwa njia ya Mwokozi. Tumekwisha kuona jinsi taifa la Waisraeli lilivyotoka kwa Ibrahimu. Musa aliliongoza taifa hili kutoka utumwani huko Misri akiwaongoza mpaka nchi ya Kanaani. Lakini, kwa sababu wanadamu walikuwa wakizidisha uovu wao, Mungu aliwapa Waisraeli zile Ami Kumi (Torati) kwa mikono ya Musa. Kazi ya Torati ilikuwa kuupunguza uovu wa watu na kuwaongoza kabla hajaja yule Mwokozi mwenyewe (Wagalatia 3:19-24). Kusudi watu wawe tayari kumpokea Mwokozi, Mungu alituma manabii wengi walioweza kutabiri mambo mengi kuhusu kuzaliwa kwake na kazi yake.
Vitabu vya Agano Jipya vinavyoitwa INJILI vinaeleza habari ya Mwokozi huyo. (injili maana yake ni HABARI NJEMA.) Vitabu vya injili ni Mathayo, Marko, Luka, na Yohana. Katika vitabu hivyo, twasikia jinsi mambo yale yaliyotabiriwa kuhusu Mwokozi yalivyotimilizwa katika YESU KRISTO. Yesu Kristo alikuja kubariki mataifa yote kama Mungu alivyomwahidi Ibrahimu. Hatutakuwa na nafasi ya kutaja moja moja mambo yote yalivyotabiriwa kuhusu Yesu bali tutachagua mambo machache tu yawe mifano.
Kwanza, tukumbuke maneno ya Mungu mwenyewe katika Mwanzo 3:15. Hapo Mungu alitabiri kwamba uzao wa mwanamke utaponda kichwa cha Shetani. Je! Kwa nini Mungu alitaja “uzao wa mwanamke” badala ya kusema “uzao wa mwanamume”? Maana, kufuatana na desturi za wanadamu wengi, mtoto anapozaliwa watu humtaja kuwa uzao wa baba yake wala sio wa mama yake. Sasa, basi, kwa nini Mungu alisema “uzao wa mwanamke” utaponda kichwa cha Shetani? Jawabu linapatikana tunaposoma mlango wa kwanza wa Mathayo. Hapo twasikia jambo la ajabu kweli kweli, maana tunaambiwa kwamba Yesu Kristo hakuzaliwa na baba wa kimwili bali alizaliwa na bikira Mariamu, aliyemzaa Yesu, alichukua mimba kwa nguvu ya Roho Mtakatifu wa Mungu kabla yeye na mposa wake hawajakaribiana. Nabii Isaya alitabiri jambo hili akisema, “Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume” (Isaya 7:14). Basi ndiyo maana Yesu alikuwa uzao wa mwanamke wala si wa mwanamume!
Maneno mengine machache ya manabii yaliyotimizwa katika kuzaliwa kwa Yesu ni kwamba atazaliwa kutokana na ukoo wa Daudi (Yeremia 23:5; Isaya 9:6-7; Mathayo 1:1). Kwamba atazaliwa katika mji wa Bethlehemu (Mika 5:2; Mathayo 2:1), na kwamba Yohana Mbatizaji atatayarisha njia yake (Isaya 40:3; Mathayo 3:1-3).
Shetani alipoona kwamba Yesu amezaliwa ili awe Mwokozi, alikuja kwake akitaka kumfanya atende dhambi. Hata ingawa Shetani alimjaribu Yesu kwa aina zote za dhambi, lakini Yesu hakutenda dhambi kamwe (Mathayo 4:1-11; Waebrania 4:14-15).
Yesu alipoanza kazi yake alizungukazunguka huko na huko kati ya Wayahudi akiwafundisha habari ya Mungu na kufanya mema kwa watu wote kama alivyotabiriwa. Mungu alimwezesha Yesu kufanya mambo mengi ya ajabu na kuponya aina zote za ugonjwa. Vipofu, viwete, wenye ukoma, viziwi, na kadhalika, wote
waliponywa na Yesu. Zaidi ya hayo, Yesu aliweza kuwafufua wafu! Mungu alimwezesha Yesu kufanya mambo hayo yote kusudi yawe ishara au dalili ya kuonyesha kwamba Yesu alitumwa na Mungu. Kwa ajili ya mafundisho na matendo ya Yesu, watu wengi walimfuata wakithibitisha kwamba yeye ndiye Mwokozi.
Kati ya wanafunzi wake, Yesu aliwachagua watu 12 wanaoitwa Mitumne (Mathayo 10:2-4). Aliwaambia watu hawa kwamba atalijenga kanisa lake (Mathayo 16:18). Vile vile, aliwaambia “Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapouona ufalme wa Mungu umekuja kwa nguvu” (Marko 9:1). Yesu liwatuma wanafunzi hawa kuhubiri kwamba ufalme wa mbinguni umekaribia. Tutajifunza zaidi kuhusu kanisa na ufalme katika somo la tano.
Hata ingawa watu wengi walimpenda Yesu, walakini walikuwapo wengine ambao hawakumwamini. Viongozi wa dini ya Wayahudi walikuwa na wivu kuona jinsi watu wengi walivyokuwa wakiondoka kwao kwenda kufundishwa na Yesu. Tena, walimkasirikia Yesu kwa sababu aliwaonyesha jinsi walivyokuwa wanafiki (maana, viongozi hawa walikuwa wakifundisha sheria za Mungu bali wao wenyewe hawakuzishika). Kwa sababu hizo, walianza kudhihaki wakisema kwamba Yesu alipata nguvu ya kuponya watu kutokana na Shetani. Basi walikuwa wakitafuta nafasi ya kumwua. Hatimaye, wakamchukua Yesu kwa nguvu, wakamleta mbele ya wakuu wao wakisema kwamba Yesu alimkufuru Mungu akijisema kuwa mwana wa Mungu. Wakuu hao wakasema kwamba Yesu alistahili kuuawa. Kwa hiyo, walimchukua nje ya mji, wakamsulibisha.
Manabii walitabiri mambo mengi sana yaliyotimilizwa katika kusulibishwa kwake Yesu. Kwa mifano: walitabiri kwamba atauawa pamoja na wakosaji, kwamba askari watapiga kura kwa nguo zake, kwamba damu yake itamwagika ingawa mifupa yake haitavunjwa, kwamba atazikwa pamoja na matajiri, kwamba atafufuliwa bila kuona uharibifu, na kwamba atapaa mbinguni katika wingu.
Kabla hajauawa, Yesu mwenyewe alitabiri kwamba atakufa na kwamba baada ya siku tatu atafufuka. Kwa sababu hiyo, adui za Yesu waliweka askari kulinda kaburi lake ili wanafunzi wasije kuondoa maiti wakisema kwamba Yesu amefufuka. Hata hivyo, katika siku ya tatu Mungu alimfufua Yesu. Mara alianza kujionyesha kwa wanafunzi wake akiwathibitishia kwamba yeye ndiye mwana wa Mungu kweli kweli. Yesu aliwaonyesha wanafunzi wake jinsi ilivyotakiwa kwamba auawe kusudi katika yeye watu waweze kumshinda Shetani na kuokolewa kutokana na dhambi. Kumbuka jinsi katika Mwanzo 3:15, Mungu alivyotabiri kwamba uzao wa mwanamke utaponda kichwa cha Shetani. Jambo hili lilitimizwa katika kifo na ufufuo wa Yesu, maana Yesu alipofufuka kutoka katika wafu alionyesha waziwazi kwamba alimshinda Shetani aliyekuwa na mamlaka juu ya mauti.
Yesu hakustahili kufa, maana yeye hakutenda dhambi yo yote. Yesu alikubali kuuawa kusudi ajifanye kuwa dhabihu iliyotolewa kwa ajili ya dhambi za wanadamu wengine. Kwa sababu ametupenda hivyo, watu wote wanaomtii Yesu wanaweza kuokolewa kutokana na adhabu ile inayokuja kwa ajili ya dhambi zao (Waebrania 5:9).
Katika kitabu cha Matendo ya Mitume twasikia jinsi wanafunzi wa Yesu walivyofundisha watu kuhusu Yesu na wokovu unaopatikana katika yeye. Mifano ya watu wengi waliookolewa, kutokana na dhambi zao inapatikana humu. Tena, twasoma habari nyingi kuhusu mwanzo wa kanisa la Kristo na jinsi lilivyoweza kuenea katika mahali pengi duniani.
Vitabu vingine 21 vya Agano Jipya ni nyaraka au barua zilizoandikwa kwa ajili ya Wakristo walioishi mahali mbalimbali. Hatuwezi kutaja mambo yote yaliyoandikwa katika nyaraka hizo bali tutataja mambo machache yaliyo muhimu. Paulo aliandika barua kwa Wakristo wa Rumi kusudi awaeleze jinsi katika Yesu Wayahudi na mataifa pia wanavyoweza kuwa na umoja na kupata msamaha wa dhambi. Aliwaandikia Wakristo wa Korintho barua mbili akiwaonya kuhusu hatari ya faraka katika kanisa na kuhusu zinaa, chakula cha Bwana, kiyama, na kutoa changizo. Aliandika barua kwa Wagalatia akiwaonyesha kwamba
Wakristo hawako chini ya sheria za Musa. Barua kwa Waefeso na Wakolosai zinafundisha kwamba Yesu ni kichwa cha kanisa lake. Katika barua zake kwa Wathesalonike, Paulo aliwaambia kwamba Yesu hatakuja mara, bali atakapokuja atawafufua wafu wote na kuwapa Wakristo walio waaminifu thawabu. Katika barua zake kwa Timotheo na Tito twajifunza kuhusu maaskofu na mashemasi wa kanisa. Katika barua kwa Waebrania twasikia jinsi Agano la Kale lilivyoondolewa wakati Yesu aliposimamisha Agano Jipya linaloweza kuwaokoa wanadamu. (Tutajifunza zaidi kuhusu agano hili katika somo la nne.) Yakobo, katika barua yake, anatuonyesha kwamba imani pasipo matendo haifai kitu. Petro aliandika barua mbili kuwafariji Wakristo walioteswa kwa ajili ya kumfuata Yesu. Yohana aliandika barua tatu akiongea habari ya upendo na kuonya kuhusu hatari ya walimu wasiofundisha ukweli. Yuda aliwaonya Wakristo wasikubali mafundisho mengine ila yale yaliyotolewa na Yesu.
Kitabu cha mwisho katika Biblia huitwa Ufunuo wa Yohana. Kitabu hiki kimejawa na maneno ya unabii, maana Yesu alimwambia Yohana mambo yatakayotendeka baadaye. Ni vigumu kuelewa mambo yote yaliyomo katika kitabu hiki kwa sababu kinatumia mafumbo na mifano mingi isiyo waziwazi. Lakini, hata ikiwa hivyo, kuna faida kubwa katika kukisoma, maana kinaonyesha kwamba watu wanaomtii Yesu wataweza kumshinda Shetani na kupewa thawabu katika mahali ambapo Yesu ameandaa kwa ajili yao. Katika mji huu wa Mungu hawataona tena njaa, uchi, maumivu, machozi, wala kitu kingine kilicho kibaya bali watakuwa na raha mno siku zote.
Katika mlango wa mwisho wa Biblia twasonma maneno yafuatayo:
“Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.” Ufunuo 22:18-19